Mwandishi wetu  Lindi

Mgombea uRais kupitia chama cha ACT-Wazalendo, Bernard Membe amesema akichaguliwa nakuwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya serikali atakayounda na kuongoza haita wabughuzi wafanyabiashara wadogo wanaonunua mazao kwa wakulima ambao katika mikoa ya Lindi na Mtwara wanatambulika kama kangomba.

Membe ametoa ahadi hiyo leo wakati wa uzinduzi wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Mpilipili, manispaa ya Lindi. Uzinduzi ambao pia ulihudhuriwa na kiongozi mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe na mwenyekiti wa taifa, Maalim Seiff Shariff Hamad.


Membe alisema serikali atakayounda na kuongoza iwapo atachaguliwa kuwa Rais haitawabughuzi wafanyabiashara hao. Kwani anatambua kwamba uchumi wa nchi zote zilizofanikiwa kiuchumi duniani unategemea wafanyabiashara wa kati. Kwahiyo atawaruhusu wananunue mazao kwa wakulima bali walipe kodi.

Alisema hata wanaonunua mazao kwa wakulima kutoka mataifa ya nje ni kangomba wa kimataifa. Kwahiyo haoni sababu ya kuwaruhusu kangomba wa ndani kununua mazao ya wakulima. Bali kubwa ni kuhakikisha wanalipa kodi.

Katika kuhakikisha azima yake hiyo inafanikiwa, Membe amejinasibu kwamba ataunda wizara ya biashara ambayo itakuwa na wajibu wa kutafuta masoko ya mazao ya wakulima. Huku akihaidi kupita katika mikoa yote kuzungumzia changamoto za kila mkoa ambazo wananchi wanakabiliana nazo ili kuwapa matumaini ya kutatua changamoto hizo iwapo atachaguliwa kuwa Rais.

" Wakulima watapeleka na kuuza mazao yao popote bila ya kuingiliwa na serikali, bali walipe kodi," Membe alisisitiza.

Aidha Membe alisema kama atakuwa Rais atapandisha mishahara ya watumishi na kuwapandisha madaraja. Kwani ni haki ya watumishi wa umma. Huku akihaidi kuwalipa fedha za likizo.

Mgombea huyo wa uRais licha ya kuhaidi hayo, lakini pia amehaidi kuimarisha ushirikiano na mataifa mbalimbali duniani. Kwamadai kwamba hivi sasa Tanzania imekuwa kama kisiwa kilichojitenga na mataifa mengine kuhusu mahusiano na ushirikiano.

Katika hatua nyingine Membe alisema anauhakika wakushinda uchaguzi. Kwani hata ndani ya Chama Cha Mapinduzi wapo wengi wanaomuunga mkono kutokana na kuchoshwa na hali ya mambo.

"Nawafurahia sana wanaCCM kwani wamechoka, wananiunga mkono. Wapo wanaosema watabaki na kadi tu," Membe alijagamba.

Uzinduzi wa kampeni za ACT- Wazalendo ulizinduliwa na mwenyekiti wa taifa wa chama hicho, Maalim Seif Shariff Hamad. Ambaye katika hotuba yake ya uzinduzi alizungumzia kitendo cha tume ya uchaguzi kuwaengua wagombea wa ubunge kupitia chama hicho. Hasa wagombea waliopo katika kisiwa cha Pemba.