NIKICHAGULIWA KUWA  MBUNGE  NITAJENGA  STANDI 


Mwandishi wetu

MGOMBEA ubunge katika Jimbo la Masasi mjini kwa chama cha Mapinduzi (CCM) Geofrey Mwambe amesema kuwa akichaguliwa kuwa mbunge wa jimbo hilo atahakikisha wilaya ya Masasi inajengwa stendi ya kisasa ya mabasi inayoendana na hadhi ya wilaya hiyo jambo ambalo litasaidia kundoa msongamano wa magari katika stendi iliyopo kwa sasa.

    Aidha,Mwambe amesema kuwa atasimamia suala la upatikanaji wa mikopo ya kiuchumi kwa vijana na wanawake na makundi mengine mbalimbali ikiwemo makundi ya watu maalumu lengo kuifanya Masasi inakuwa ya kisasa kama wanavyohitaji wanamasasi.

  Mwambe aliyasema hayo jana mjini Masasi alipokuwa akizungumza na mamia ya wananchi wa wilaya ya Masasi kwenye uzinduzi wa kampeni zake za kuomba ridhaa kwa wananchi wa jimbo hilo yakutaka achaguliwe kuwa mbunge wa jimbo hilo.

   Alisema anatambua kuwa wakazi wa wilaya ya Masasi hasa walioko katika jimbo hilo wanakiu kubwa ya kuona maendeleo yanapatikana na yanawanufaisha wananchi hasa kiuchumi, kijamii na kisiasa.

   Mwambe alisema anavipaumbele mbalimbali ambavyo anatarajia kuwaeleza wananchi wa jimbo hilo vipaumbele ambavyo kama wananchi hao watamchagua kuwa mbunge katika jimbo hilo ayavitekeleza kwa vitendo na kwamba Masasi itapiga hatua kubwa ya kimaendeleo.

    Alisema kipaumbele cha kwanza ambacho ataanzanacho akiwa mbunge ni ujenzi wa stendi ya mabasi ambayo itakuwa ya kisasa na hiyo inatokana na Masasi kutokuwa na stendi iliyobora kwa sasa na stendi hiyo itakayo jengwa itaendana na hadhi ya Masasi.

  “Mkinichagua kuwa mbunge wa jimbo hili kwanza tutajenga stendi ya kisasa ya mabasi na hii itakuwa stendi bora sio tu ndani ya mkoa wa Mtwara bali Tanzania mzima…mimi nimefanya makubwa nikiwa katika ngazi nyingine za uongozi hivyo siwezi kushindwa kuionoza Masasi pekee yake,”alisema Mwambe 

  Mwambe alisema lipo suala la uchumi kwa vijana na wanawake bado limekuwa ni tatizo sugu kwa vijana wengi kwa sababu vijana hao wamekuwa wakikosa fursa ya kupata mikopo ya kiuchumi lakini iwapo atachuguliwa kuwa mbunge atahakikisha kundi hilo linapatiwa mikopo ya kiuchumi yenye riba nafuu.

    Aidha,Mwambe aliongeza kuwa atahakikisha anasimimia suala la upatikanaji wa huduma za afya hasa wananchi waishio maeneo ya vijijini ambao utembea umbali mrefu kwenda katika hospitali ya halmashauri ya mji Masasi kufuata matibabu ambapo atahakikisha kila kijiji kunakuwepo na Zahanati na huduma zinazotolewa kwa ufanisi.

    Awali akimkaribisha mgombea ubunge huyo, mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mtwara, Yusuf Mnanila alisema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita serikali ilitoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa ajili ya wakazi wa Masasi.

   Alisema jumla ya fedha ambazo serikali imeshazitoa kutelekeza miradi ya maendeleo ni katika miaka hiyo mitano iliyopita ni sh.4.4 bilioni kutekeleza baadhi ya miradi ambayo ni elimu, katika shule ya Chiungutwa sekondari ilipatiwa sh.578 milioni, sekondari ya Lupaso sh.400 milioni, Ndanda sekondari ujenzi wa bwalo la chakula sh. 600 milioni, Kitunda uejenzi wa shule ya mfano sh.700 milioni 

   Alisema wananchi waendelee kuwa na imani na serikali yao na kwamba ikifika oktoba 28 mwaka huu,2020 siku ya kupiga kura wakachaguwe viongozi wanaotokana na chama cha mapinduzi ili waweze kuendelea kuwaletea maendeleo wanayoyatamani wanamasasi